Maelfu ya watu Jumapili walikusanyika katika uwanja wa mchezo wa raga katika mji wa Bloemfontein Afrika Kusini kusherehekea miaka mia moja ya chama tawala African National Congress- ANC.

Sherehe  hizo ambazo zimehutubiwa na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma  zimehitimisha sherehe mbalimbali  za mwishoni mwa wiki  kwa heshima ya chama  kikongwe barani Afrika  kilichokuwa chanzo cha kupigania ukombozi.

Saa sita usiku kuamkia Jumapili saa za Afrika Kusini rais Zuma aliwasha mwange katika kanisa la Bloemfontein ambapo wasomi weusi na wanaharakati walizindua chama hicho cha ANC Januari 8 mwaka wa 1912. Dazeni ya viongozi kutoka nchi nyingine za Afrika walihudhuria sherehe hizo kukitambua chama cha ANC ambacho  kiliongozwa na rais mstaafu Nelson Mandela  baada ya kutimuliwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Bwana Mandela hata hivyo hakuhudhuria sherehe hizo kwa sababu afya yake imedhoofika. Chama cha ANC kilianzishwa kupigana dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kupata ushindi mwaka wa 1994 kilipotimua utawala wa wazungu waliokuwa wachache huko Afrika Kusini. Nelson Mandela alikuwa rais wa kwanza mweusi nchini humo.