Muda wa kuhudumu kwa serikali ya mpito ya Somalia –TFG unakatika mwezi Agosti mwaka huu. Na kutokana na ugumu uliopo wa kuweza kuandaa uchaguzi mkuu katika mazingira ya machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe viongozi wa Somalia na wale wa kimataifa  walikamilisha mkutano Jumamosi kwa makubaliano  ya kuunda mpango wa kuteuwa serikali mpya katika muda wa miezi sita ijayo. Mjumbe  maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia balozi Augustine Mahiga  alisema mkataba uliofikiwa katika mji wa Garowe utaleta utawala halali na unaohitajika sana Somalia. Mpango mpya  wa kuunda serikali mpya na halali ya Somalia utakuwa na viti 1000 vya bunge ifikapo mwezi Aprili. Wabunge hao  watachaguliwa kutoka mashinani  na miongoni mwao kutakuwa na wanawake , wazee , viongozi wa kidini  wasomi na Wasomali wanaoishi nje ya nchi. Wabunge watakaoteuliwa  wanatazamiwa kuanza kazi zao bungeni mwezi mei na watamchagua spika ifikapo Juni na rais mwezi julai. Balozi Mahiga  alisema kundi la wanamgambo wa kiislam lenye msimamo wa kadri pia litajumwishwa kwenye mkusanyiko huo wa kisiasa. Idadi ya viti bungeni itapunguzwa kutoka 550 hadi 225. Balozi  Mahiga alieleza furaha yake kwamba chini ya makubaliano mapya asili mia 30 ya viti vya bunge vitakuwa vya wanawake na hivyo kuongeza idadi  ya uwakilishi wa wanawake katika bunge la Somalia kwa asilimia 12.5. Mjumbe huyo maalum  wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia atakwenda London, ambapo Alhamis wiki hii, serikali ya Uingereza imeandaa kongamano kubwa kujadili hali ya baadaye ya Somalia .