Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton  amekwenda Libya Jumanne katika ziara ya kushtukiza na kukutana na viongozi wapya nchini humo huku wapiganaji wa serikali ya muda wakiendelea kupigana na wanajeshi watiifu kwa  kiongozi wa zamani Moammar Ghadafi. Waziri Clinton aliwasili Tripoli leo Jumanne ambapo ameahidi msaada mpya  wa mamilioni ya dola  utakaotumiwa kwa program za elimu na afya kwa wapiganaji waliojeruhiwa katika vita nchini humo. Fedha hizo pia zitatumiwa  kuharibu  maelfu ya makombora  ili kuyazuia kufikia wanamgambo. Maafisa wa Marekani wanasema msaada wake kwa Libya tangu mzozo kuibuka nchini humo umefikia dola milioni 135. Waziri Clinton alikutana na kaimu waziri mkuu  Mahmud Jibril na mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la mpito Mustafa Abdel Jalil wakati wa zaiara yake. Ni afisa wa kwanza wa ngazi ya juu  kutoka Marekani kwenda Tripoli tangu maasi kuanza dhidi ya Ghadafi mwezi Februari.