Afisa wa Kenya anasema majeshi ya nchi hiyo yamefanya mashambulizi ya angani kusini mwa Somalia na kuuwa dazeni ya wanamgambo wenye ushirika na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida katika juhudi zinazoendelea kutokomeza wanamgambo nchini Somalia. Msemaji wa jeshi kanali Cyrus Oguna, aliwaambia waandishi habari  Jumamosi kuwa wanamgambo wapatao 60 wa kundi la al-Shabab waliuawa   Ijumaa katika mji wa Garbaharey katika eneo la Gedo huko Somalia. Alisema majeshi ya Kenya yalipashwa habari juu ya eneo walilokuwa wanamgambo hao na kisha kuwashambulia. Anasema idadi ya waliouawa inategemewa kuongezeka. Majeshi ya  Kenya yaliingia Somalia  mwezi Oktoba kupambana  dhidi ya kundi la  al –Shabab linalodhibiti eneo kubwa na kusini na katikati mwa Somalia  na ambalo Kenya inalaumu kwa utekaji nyara ndani ya ardhi yake na kwenye mpaka baina ya nchi hizo mbili.  Habari kutoka Uingereza zimesema leo Jumamosi kuwa London inaamini Kenya inakabiliwa na tishio la kushambuliwa na magaidi. Ofisi inayohusika na maswala ya nje  huko London, inasema uingereza inaamini kuwa magaidi wamo katika hatua za mwisho  mwisho za kupanga njama za kuishambulia Kenya.