Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon Panetta amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya daktari wa Pakistan aliyesaidia Marekani kumpata  kiongozi wa kundi la kigaidi Osama Bin Laden. Waziri Panetta alisema  katika kipindi cha 60 Minutes cha kituo cha  televisheni cha CBS kwamba  Dr. Shikal Afridi alitoa habari za kijasusi zilizosaidia majeshi ya Marekani kumkamata na kumwua gaidi Osama Bin Laden tarehe 2 mwezi Mei mwaka jana katika mji wa Abbottabad. Mahojiano na waziri huyo wa ulinzi yatapeperushwa hewani Jumapili. Pakistan imemkamata Dr. Afridi na kumshtaki kwa kosa la uhaini. Daktari huyo aliyekuwa akifanyia marekani kazi za kijasusi, aliongoza program ya utoaji chanjo ili kupata DNA iliyothibitisha kuwepo kwa Bin Laden katika uwanja aliokutwa na kuuliwa huko Abbottabad. Bwana Panetta amesema  hatua ya Pakistan ya kumkamata mtu aliyesaidia kumnasa gaidi kama huyo ni makosa makubwa. Waziri huyo wa ulinzi wa Marekani amesema  anaamini kuwa kuna mtu  katika mamlaka ya Pakistan aliyejua fika mahali Bin Laden alikuwa akijificha.