Serikali ya Somalia imetoa wito wa kumalizika kwa marufuku ya silaha nchini humo, ili iweze kupambana vizuri zaidi  na kundi la wanamgambo wa kiislam la Alshabab. Taarifa ya serikali Jumatatu imesema muungano wa Alshabab na al qaida uliotangazwa wiki iliyopita utaongeza wasi wasi juu ya hali ya kiusalama nchini Somalia. Imesema Somalia inaweza kuwa ngome ya mtandao wa kigaidi. Serikali imesema ingependa kuona kuondolewa kwa  marufuku ya kuingiza silaha nchini humo iliyowekwa na Umoja wa Mataifa  mwaka 1992 baada ya serikali ya mwisho ya Somalia iliyogubikwa na  utata kuanguka na nchi kutumbukia kwenye  ghasia.