Moja ya vyama vikuu vya wafanyakazi  nchini Afrika Kusini kimekataa pendekezo jipya la nyongeza ya mishahara kutoka kwa  serikali  ili kumaliza mgomo wa wiki mbili.

Chama chenye wanachama laki 2 cha National Education Health and Allied workers kimekataa pendekezo hilo baada ya mazungumzo na wawakilishi wa serikali Jumatano. Makundi mengine hayajatangaza uamuzi wao.

Lakini pendekezo hilo jipya la serikali limepelekea chama cha wafanyakazi wa migodi kuacha  mgomo uliokuwa umepangwa kufanyika Alhamis. Chama hicho cha wafanyakazi kilisema kimesitisha mgomo huo ili kuwapa wafanyakazi wa serikali muda wa kufanya maamuzi mapya  juu ya pendekezo hilo.

Pendekezo jipya la serikali lilikuwa  la  kuongeza mshahara kwa  asilimia 7.5 na marupurupu ya  nyumba ya dola 109.  Vyama vya wafanyakazi wa umma vilidai nyongez  ya asilimia 8.6 na pamoja na  posho la nyumba.

Mgomo huo wa wafanyakazi wa umma wapatao milioni 1.3 umepelekea kufungwa kwa  shule na wanajeshi  kuagizwa kuchukua udhibiti wa hospitali  za umma.

Wafanyakazi wengine wa viwanda vya kutengeneza na kukarabati magari  walianza mgomo jumatano wakidai nyongeza ya asilimia 15 ya mshahara..